Timu
ya Azam FC ya Dar es Salaam, imenyang'anywa ushindi wa pointi tatu na
mabao matatu uliyoupata katika mechi Na. 156 ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.
Uamuzi huo umetokana na Azam kumtumia mchezaji Erasto Nyoni kwenye
mechi hiyo wakati akiwa na kadi tatu za njano. Mchezo huo ulifanyika
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 37(4) ya Ligi Kuu Toleo la
2015 inayoelekeza kuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika
michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata wa timu yake. Hivyo
kwenda kinyume na Kanuni husika.
Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) ya Ligi Kuu Toleo la 2015, timu
ya Mbeya City imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Kadhalika Bodi ya Ligi imelionya Benchi la Ufundi la timu hiyo
kuongeza umakini katika utunzaji wa kumbukumbu za kadi za wachezaji
wake. Pia imezikaribisha timu zote wakati wowote kuomba kumbukumbu
zozote kila zinapozihitajika.
No comments:
Post a Comment